Monday 12 September 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA PILI KATIKA KOZI ZA CHETI NA DIPLOMA KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017

TAARIFA KWA UMMA 

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linapenda kuwaarifu wote walioomba kudahiliwa katika kozi mbali mbali za cheti na diploma na Umma kwa ujumla kuwa uhakiki wa uteuzi wa awamu ya pili kwa waombaji wa cheti na diploma umekamilika na kwamba uteuzi huu sasa unaonekana kwenye kurasa binafsi (profile) za waombaji. Hii ina maana kuwa waliochaguliwa sasa wanaweza kuona mahali walipochaguliwa kupitia kurasa zao binafsi.
Hata hivyo, Baraza linaomba radhi kwa kuwa uhakiki wa uteuzi kwa baadhi ya vyuo haujakamilika hivyo Baraza litashindwa kuwaonyesha waombaji wa vyuo hivyo uteuzi wao. Vyuo hivyo ni pamoja na vyuo vya kilimo na uvuvi na baadhi ya vyuo vikuu.
Baraza pia linapenda kuwaarifu waombaji waliofanya maombi kwenye vyuo vya Ualimu vya Serikali kuwa uteuzi kwenye vyuo hivyo bado unasubiri mwongozo wa Serikali na hivyo watafahamishwa mara Baraza litakapopata mwongozo kutoka Wizara yenye dhamana ya Elimu juu ya uchaguzi huo.
Imetolewa na
Ofisi ya Katibu Mtendaji
NACTE
Tarehe: 10 Septemba, 2016
Share:

Thursday 1 September 2016

TAHADHARI KWA WAKUU WA VYUO, WADAU NA UMMA KWA UJUMLA


TAARIFA KWA UMMA 

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linatoa tahadhari kwa Wamiliki na Wakuu wote wa Vyuo vya Elimu ya Ufundi nchini kuwa kumeibuka matapeli wanaowaomba fedha au rushwa wakuu wa vyuo hasa vilivyopewa notisi na Baraza ya kushushwa hadhi au kufungiwa ili kuweza kuwasaidia kutatua matatizo yao kupitia namba mbalimbali za simu wanazozitoa.

Baraza linaendelea na kuwatahadharisha wateja wetu kuwa msikubali kupokea simu zenye kuwaomba fedha au kutoa kitu chochote wakati mnapotekeleza maelekezo ya Baraza au hata baada ya kutekeleza maelekezo hayo.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza anatoa tahadhari hii baada ya ofisi yake kupokea malalamiko hivi karibuni kutoka kwa baadhi ya Wakuu wa Vyuo na Wamiliki ambao wamedai kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kuwa Maafisa wa NACTE na kuwadai kiasi cha fedha kama masharti ya kutatuliwa matatizo yao. Pia Baraza limepokea taarifa kutoka kwa Wadau wanaolalamika kuwa kuna kundi la watu wanaodai kupewa fedha ili wasaidiwe kupangiwa vyuo fulani vya ufundi kwa masomo mbali mbali.

Baraza halina utaratibu wa kuomba fedha au zawadi ya aina yeyote kwa Mkuu wa Chuo au Mtu yoyote kama sharti la kupata huduma/msaada fulani.

Ni imani yetu kwamba wakati Baraza likiendelea na uchunguzi wa kuwabaini matapeli hao ili kuwachukulia hatua za kisheria, Wadau wetu wataongeza umakini na kuchukua tahadhari binafsi na watu wa namna hiyo.


Imetolewa na
Ofisi ya Katibu Mtendaji – NACTE


01 Septemba, 2016.
Share: