Sunday 27 July 2014

Ubadilishaji wa Combination kwa Form Five 2014


WANAFUNZI WALIOFAULU SAYANSI



Ni kwa wale waliofaulu vizuri masomo ya sayansi na kupangiwa masomo ya sanaa
Katibu Mkuu Tamisemi Ndugu Jumanne Sagini akiongea na waandishi wa habari katika 
mkutano uliofanyika ofisi ndogo za wizara zilizopo Magogoni Dar es Salaam
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa an Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Ndugu Jumanne Sagini, amesema kuwa wanafunzi wote waliofaulu vizuri masomo ya sayansi na wanapenda kusoma masomo hayo lakini walipangiwa masomo ya sanaa kutokana na kukosa nafasi, wanayo fursa ya kubadilisha kupitia kwa wakuu wao wa shule; na endapo kwenye shule walizopangwa hakuna tahasusi za masomo ya Sayansi wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa Maafisa elimu Mikoa ambapo shule hizo zipo, kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa, ili waweze kubadilishiwa tahasusi za sayansi kwenye shule zilizopo kwenye Mikoa husika.
Ngugu Jumanne Sagini aliyasema hayo katika mkutana na waandishi wa habari uliofanyika tarehe Julai 22, 2014 katika Ofisi za OWM-TAMISEMI, Dar es Salaam.
“Tumetoa maagizo kwa wakuu wa shule na maofisa Elimu wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha wanafunzi waliofaulu masomo ya sayansi na kupangiwa sanaa wanabadilishiwa iwapo watataka.” Alisema ndugu Jumanne Sagini.
Aidha ndugu jumanne Sagini alisema kuwa Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi kusoma masomo hayo, imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati. Pia, Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kwa wanafunzi waliobaki kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za kidato cha tano, baada ya kubaini uwepo wa nafasi hizo; na inatarajiwa kwamba baadhi ya wanafunzi wenye sifa watachaguliwa kwenda kusomea ualimu na vyuo vingine vya ufundi.
Katika matokeo ya mtihani kwa mwaka 2014, inaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 22,685 kati yao Wasichana 7,859 na Wavulana 14,826 wamechaguliwa kusoma tahasusi za sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746 kati yao Wasichana 5,038 na Wavulana 13,708 kwa mwaka 2013. Aidha tofauti na miaka mingine iliyopita, Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I -III umeongezeka kutoka watahiniwa 35,357 mwaka 2012 hadi 71,527 mwaka huu. Ufaulu huu ni zaidi ya asilimia mia moja ya watahiniwa waliokuwa na sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka 2013.
“Natoa pongezi nyingi kwa walimu, wanafunzi,wazazi/walezi na wadau wote wa elimu kwa juhudi walizozifanya kuwezesha ufaulu katika masomo ya sayansi kuongezeka kwa kiasi cha kuridhisha.” Alisema ndugu Jumanne Sagini. 
Pia ndugu Jumanne Sagini alieleza kuwa matokeo haliyotangazwa mwaka huu 2014 yanakaribia sana malengo ambayo Serikali imejiwekea kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (yaani Big Results Now-BRN) ambapo serikali ilijiwekea lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa asilimia 60 mwaka 2013. Matokeo halisi yanaonyesha kuwa ufaulu umepanda kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.
Wakati huohuo shule zote zilizofanya vibaya katika matokeo ya Kidato cha Sita mwaka huu 2014, ambapo mazingira na nafasi yake iliruhusu kufanya vizuri, zimeamriwa kujieleza sababu za kufanya vibaya.
Ndugu Jumanne Sagini alisema kuwa Makatibu Tawala Mkoa wameagizwa kutoa maelezo na kufanya utafiti ndani ya mwezi kubaini sababu ya shule hizo kufanya vibaya ili hatua stahiki zichukuliwe, hali hiyo isijirudie.
“Tumetaka maelezo kutoka kwa Makatibu Tawala Mkoa; kwa nini shule zimefanya vibaya. Matokeo ya hovyo kama haya ni jambo lisiloweza kueleweka; na wasimamizi wa elimu nimewaambia halikubaliki.” Alsema ndugu Sagini.
Aidha ndugu Sagini aliendelea kusema “Shule kongwe kama Tambaza na Iyunga, zinazopewa fedha na Serikali, zina walimu wa kutosha, zina maabara, nyumba za walimu lakini bado matokeo yanakuwa ya hovyo, tunataka kujua sababu”.
Ndugu Sagini aliendelea kusema: “Sisi wenyewe imetuudhi, imetuhuzunisha na kwa kweli haikuwa matarajio ya Serikali kwa shule kongwe kuwa na matokeo mabaya”.
Hata hivyo alisema kuwa anazo taarifa za kuwepo kwa vikao vya kushughulikia matokeo mabaya katika shule ya sekondari Tambaza iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha aliainisha kuwa tatizo lililochangia baadhi ya shule kufanya vibaya ni kukosa usimamizi makini, hivyo aliwataka wakuu wa shule kutimiza wajibu wao.

















Share:

0 comments:

Post a Comment