JESHI
LA KUJENGA TAIFA
TAARIFA KUHUSU VIJANA WALIOHITIMU MAFUNZO YA JKT KWA
KUJITOLEA NA KUDAI KUAJIRIWA NA SERIKALI
Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa Julai
10, 1963 na serikali kwa lengo la kuwaweka pamoja vijana wa nchi hii na kuwapa
malezi kuhusu uzalendo na umoja ili kuondoa dalili za matabaka zilizoanza
kujitokeza katika jamii baada ya uhuru.
Baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa JKT ni:
•
Kubadili
fikra za vijana wa nchi hii kutoka ile hali ya ukoloni kutegemea nchi nyingine
kuleta maendeleo.
·
Kukusanya
nguvu za vijana wote wa nchi hii na kuzielekeza kwa umoja wao kufanya kazi
pamoja kwa manufaa ya taifa.
•
Kuwafunza
vijana kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa, ili kulinda uhuru wa Taifa lao.
Jeshi la Kujenga Taifa linaunganisha
vijana bila kujali itikadi zao, dini, elimu, jinsia na mali ili kuwalea kuwa
wazalendo kwa taifa lao na kupenda kuitumikia nchi yao.
Pamoja na dhana ya kufunzwa uzalendo,
pia stadi mbalimbali za kazi hufundishwa kwa vijana hao ili waweze kujiajiri,
pindi wamalizapo mkataba yao ya kujitolea kwa miaka miwili.
Serikali ilirejesha mafunzo ya Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana wa kujitolea mwaka 2001, baada ya kusitishwa
mwaka 1994.
Masharti ya
Kujiunga na JKT kwa vijana wa Kujitolea
Kijana kabla ya kujiunga na JKT hutakiwa
kuyajua masharti na kuzifahamu taratibu za kujiunga na kuelewa kuwa JKT halitoi ajira.
Moja ya kipengele cha masharti ya
kujiunga na JKT kinasema kuwa ‘Kwa
kipindi chote nitakachokua ndani ya Jeshi la Kujenga Taifa nitakuwa nafanya
mafunzo ya kijeshi na ya stadi za kazi na maisha, na baada ya mkataba nitarejea
nyumbani. Hivyo sitalidai Jeshi la Kujenga Taifa ajira, wala kulitaka linitafutie
ajira/kazi’.
Kipengele hiki kinaainisha masharti ya
makubaliano kati ya Jeshi la Kujenga Taifa na kijana kabla ya kujiunga na
kupatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.
Aidha, Mheshimiwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na
viongozi wengine mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza kuwa, JKT halitoi ajira.
Lakini hivi karibuni wakati nchi
inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka huu, umezuka mtindo wa
makundi ya vijana waliopitia JKT katika Operesheni mbalimbali kuomba kuandamana
kwenda Ikulu kudai ajira.
Madai yanayopingana na dhana ya JKT na
kauli ya Mhe. Rais kuwa Jeshi la Kujenga Taifa haliajiri, bali vijana hujiunga
kwa hiari kwa kujitolea na baada ya mkataba wa miaka miwili wanatakiwa kurejea
walikotoka.
Aidha, Mhe. Rais
Kikwete, amewahi kutoa agizo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, taasisi za Serikali
na kuziomba zile zisizo za kiserikali kutoa ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya
JKT kulingana na sifa za kijana na nafasi zilizopo.
Takwimu zinaonesha kuwa tangu
kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT mwaka 2001 hadi mwaka jana, jumla ya vijana 104,594 wamejiunga na JKT wakiwemo
wavulana 76,832 na wasichana 27,762.
Katika kipindi hicho, jumla ya
operesheni 13 katika mafunzo ya JKT zimefanyika,
Operesheni hizo ni pamoja na Operesheni
Mkapa mwaka 2001, Miaka 40 ya JKT
mwaka 2002, Utandawazi mwaka 2004 na
Operesheni Jiajiri mwaka 2005.
Zingine ni pamoja na Kasi Mpya mwaka 2006, Maisha Bora mwaka 2007, Uadilifu mwaka 2008, Kilimo Kwanza mwaka 2009 na Operesheni Uzalendo mwaka (2010), Miaka 50 ya Uhuru (2011), Sensa mwaka 2012, Miaka 50 ya JKT (2013) na Miaka
50 ya Muungano (2014).
Vijana wa Kujitolea
walioajiriwa
Tangu mwaka 2003 hadi 2014 jumla ya
vijana 24,708 wameajiriwa katika
vyombo vya ulinzi na usalama ambapo
vijana 21,977 wakiwemo wavulana 17,307 na wasichana 4,670 wameajiriwa na Jeshi la wananchi
wa Tanzania (JWTZ).
Jeshi la Polisi vijana 3,965 wavulana wakiwa 2,943 na wasichana 1,022, Magereza vijana 2,139
wavulana 2,044 na wasichana ni 95, Zimamoto vijana 100 wavulana wakiwa ni 78 na wasichana
ni 22 na taasisi zingine vijana 592
Vijana 1,622 wameajiriwa katika taasisi mbalimbali kama TANAPA, GEITA GOLD
MINE, BANDARI na AFRICAN GOLD MINE.
Ni vema vijana hao wakatambua kuwa
tatizo la ajira sio kwao peke yao, ni tatizo la ulimwengu mzima Tanzania
ikiwemo, wanashauriwa kutumia stadi za kazi kujiajiri wenyewe.
Aidha, vijana hao watambue
kuwa walikula kiapo cha UTII, wakati
wa kuhitimu mafunzo ya JKT, hivyo suala la kuandamana ni kinyume cha kiapo
chao. Vijana hao walitumikia Jeshi la Kujenga Taifa Operesheni za nyuma na
kumaliza mkataba wa miaka miwili. Shinikizo lao la kulazimisha ajira kwa
kuandamana ni kinyume cha sheria za nchi.
Kwa
maelezo ya hapo juu utaona kuwa Jeshi la Kujenga Taifa, halina dhamana ya
kuajiri bali kufunza vijana wa taifa hili umoja, stadi za kazi na uzalendo
baada ya hapo wenye sifa za kuajiriwa hupata ajira katika taasisi mbalimbali za
serikari na binafsi.
Taarifa
hii Imetolewa na Makao Makuu
ya
Jeshi la Kujenga Taifa.
0 comments:
Post a Comment