Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB) leo imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo ya elimu ya
juu kwa muda wa miezi miwili na kusisitiza kuwa maombi yote yatapokelewa
kwa njia ya mtandao.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw.
Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema leo jijini Dar es salaam wakatik
akifungua rasmi kuwa mtandao wa kuwasilisha maombi ya mkopo
(www.olas.heslb.go.tz) utakuwa wazi kuanzia Mei 10, 2018 hadi Julai 15,
2018 ili kuwapa fursa wanafunzi wahitaji kuwasilisha maombi yao.
“Mwaka
jana tulitoa mwezi mmoja, mwaka huu tumetoa muda zaidi ili kuwawezesha
kusoma mwongozo kwa makini na kuzingatia maelekezo tunayoyatoa,” amesema
Bw. Badru katika mkutano na wanahabari ambapo pia alizungumzia mambo
muhimu yaliyomo kwenye mwongozo unaojumuisha sifa na taratibu za utoaji
mikopo kwa mwaka 2018/2019. Mwongozo huo unapatikana katika lugha za
Kiswahili na Kiingereza kwenye tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz)
Mambo muhimu yaliyomo kwenye Mwongozo
Mkurugenzi
Mtendaji amesema kuwa katika utoaji mikopo kwa mwaka 2018/2019,
kipaumbele kitatolewa kwa watanzania wahitaji wanaosoma kozi zenye
uhitaji mkubwa zaidi kitaifa kama walimu wa masomo ya sayansi na
hisabati; na sayansi ya afya ya binadamu.
“Tutatoa kipaumbele pia
kwa waombaji mikopo watakaodahiliwa katika kozi zinazohitajika
kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi wa aina zote; kozi
za sayansi za kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi na
nishati,” amesema Bw. Badru katika mkutano huo uliohudhuriwa na
wawakilishi wa wadau wa HESLB kama Shirikisho la Serikali za Wanafunzi
wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO); Wakala wa Usajili, Ufilisi na
Udhamini (RITA) na Shirika la Posta (TPC).
Aidha, ameongeza kuwa
watanzania wahitaji ambao ni yatima na wana nakala za vyeti vya vifo
vilivyothibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) nao
watapewa kipaumbele bila kujali kozi wanazosoma. Wengine watakaopewa
kipaumbele ni waombaji wenye ulemavu uliothibitishwa na Mganga wa Mkoa
au Wilaya na waombaji mikopo ambao walifadhiliwa katika masomo yao ya
stashahada (diploma) au sekondari na wana barua za uthibitisho kutoka
taasisi zilizowafadhili.
Bajeti na idadi ya watakaopata mikopo kwa 2018/2019
Kuhusu
malengo ya utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019, Bw. Badru
amesema Bodi imepanga kutoa mikopo kwa jumla ya wanafunzi wapya 40,000
na wanaoendelea zaidi ya 80,000. Kati yao, wanawake watakuwa asilimia 35
(14,000) na wanaume asilimia 65 (26,000). Bajeti ya fedha za mikopo kwa
mwaka 2018/2019 ni TZs 427 bilioni.
Maboresho yanayoendelea
Kuhusu
uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA, Bw. Badru amesema Bodi ya Mikopo kwa
kushirikiana na Kitengo cha Kompyuta cha Chuo Kikuu cha Dar es salaam
(UCC) wanaendelea na maboresho makubwa ili kuifanya mifumo ya utoaji na
urejeshaji mikopo kuwa rafiki zaidi kwa wateja. Kazi hiyo inatarajiwa
kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.
“Kwa mfano, mfumo wa
kuwasilisha maombi sasa umeboreshwa na kuwa rafiki zaidi kwa kuwa
unamwongoza mwombaji katika kila hatua – na hatoweza kwenda hatua
inayofuata kabla ya kukamilisha hatua ya awali,” amesema Bw. Badru.
Aidha,
kwa mara ya kwanza, Bodi imetoa mwongozo wake wa uombaji mikopo katika
lugha ya Kiswahili pamoja na kitabu chenye maswali na majibu 21 kuhusu
sifa na utaratibu (hatua kwa hatua) wa kuwasilisha maombi ya mikopo.
Kitabu na mwongozo vinapatikana katika tovuti ya Bodi na vitasambazwa
kwa wadau kuanzia wiki ijayo ambapo maafisa wa Bodi watatembelea shule
na waombaji nchini kote.
Maoni ya TAHLISO
Akiongea
katika mkutano huo, Meneja Usajili wa RITA Bi. Patricia Mpuya
amewahakikishia waombaji wa mikopo kuwa vyeti vya vifo na kuzaliwa
ambavyo vitawasilishwa kwa taasisi hiyo kuwa vitahakikiwa ndani ya siku
tatu.
“Tunawakumbusha kuhakikisha wanaleta maombi haraka badala
ya kusubiri ‘deadline’ (muda wa mwisho) na sisi tumejipanga wanapata
majibu ya uhakiki ndani ya siku tatu tangu tuyapokee,” amesema Bi.
Mpuya.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shirika Posta (TPC) Bw.
Hassan Mwangombe, ambao watapokea na kusafirisha kwenda HESLB fomu za
maombi ya mikopo, amesema wamejipanga kutoa huduma za elimu kwa waombaji
na intaneti katika vituo vyao zaidi ya 180 nchini. Aidha, wameandaa
bahasha maalum ambayo mwombaji mkopo atajaza taarifa zake muhimu ili
kurahisisha uwasilishaji wa maombi hayo kwa HESLB.
Mwenyekiti wa
TAHLISO Bw. George Mnali amezitaka RITA na TPC kuhakikisha wanatekeleza
mipango yao ya kuwahudumia waombaji mikopo kama walivyoahidi na kuongeza
TAHLISO itatumia muda wa miezi miwili kuwaelimisha wanafunzi wasio na
mikopo lakini wana sifa kuomba na kufuata maelekezo ya Bodi.
Wito
Bodi
imewataka waombaji mikopo kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na wale
ambao wana uwezo wa kugharamia elimu ya juu kutoomba mkopo ili kutoa
fursa kwa wahitaji halisi wengi zaidi kuomba na kupata mikopo.
HESLB
ilianza kazi rasmi mwaka 2005 ili, pamoja na majukumu mengine, kutoa
mikopo ya elimu ya juu kwa watanzania wahitaji na wenye sifa na
kukusanya mikopo iliyoiva ambayo ilitolewa na Serikali tangu mwaka
1994/1995.
Imetolewa na:
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM
Alhamisi, Mei 10, 2018