Thursday 2 November 2023

WANAFUNZI WALIOPOKEA MKOPO HESLB AWAMU YA PILI 2023/2024

 Tunapenda kuwafahamisha wanafunzi walioomba mkopo kwa mwaka wa masomo 2023-2024, pamoja na umma kuwa leo (Ijumaa, Oktoba 27, 2023) tumetangaza Awamu ya Pili (Batch II) ya wanafunzi 14,428 wapya waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 44.2 bilioni.

Wanafunzi wote waliomo kwenye awamu ya pili ni wapya wanaojiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu mbalimbali zilizopo nchini.

Idadi ya wanafunzi waliopangiwa mkopo hadi sasa

Hivyo, hadi sasa, jumla ya wanafunzi 70,560 wapya wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 203.9 bilioni. Itakumbukwa, wanafunzi 56,132 wa Shahada ya Kwanza walipangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 159.7 bilioni katika Awamu ya Kwanza (Batch I) ilitangazwa wiki iliyopita, Ijumaa, Oktoba 20, 2023.

Aidha, kati ya wanafunzi 70,560 waliopangiwa mikopo hadi sasa, wanafunzi wa kiume ni 40,470 (57.3%) na wa kike ni 30,090 (42.6%).

Utaratibu wa kupata taarifa zaidi za mkopo
Wanafunzi waliopangiwa mikopo katika Awamu ya Pili, kama ilivyo kwa waombaji wote, wanapata taarifa zaidi kuhusu mikopo waliyopangiwa kupitia SIPA - Student’s Individual Permanent Account - ambazo walitumia kuomba mkopo.

Tunawakumbusha waombaji mkopo kuwa SIPA ndiyo sehemu muhimu ya kupata taarifa za mwombaji kuhusu ombi lake la mkopo.


Orodha ya Awamu ya Tatu
Awamu ya Tatu (Batch III) ya mwisho itatolewa kabla ya Novemba 03, 2023 baada ya kukamilishwa uchambuzi wa mwisho wa maombi unaoendelea. Baada ya Awamu ya Tatu, waombaji mkopo watapata fursa ya kuwasilisha rufaa ili kufikiriwa kupangiwa mkopo au kuongezewa baada ya kuwasilisha nyaraka za ziada.

Bajeti ya fedha za mikopo kwa 2023-2024


Serikali imetenga TZS 731 bilioni kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza kwa 2023/2024 kwa ajili ya wanafunzi 220,376. Kati yao, wanafunzi 75,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza.

Share:

0 comments:

Post a Comment