Saturday, 27 August 2016

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA PILI NA KUONGEZWA KWA MUDA WA KUFANYA MAOMBI KATIKA KOZI ZA CHETI NA DIPLOMA KWA MWAKA WA MASOMO 2016/2017

 TAARIFA KWA UMMA  TAARIFA KWA UMMA 

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linapenda kuwaarifu wote walioomba kudahiliwa katika kozi za cheti na diploma na umma kwa ujumla kuwa lilifunga dirisha la maombi mnamo tarehe 15 Agosti 2016 ili kuruhusu uteuzi wa awamu ya pili kwa waombaji wa kozi hizo. Uteuzi wa awamu ya pili kwa waombaji wa cheti na diploma unatarajiwa kutangazwa tarehe 31 Agosti 2016.


Baraza pia linapenda kutoa taarifa  kuwa Mfumo wa Pamoja wa Udahili (CAS) utafunguliwa tena tarehe 1 Septemba 2016 hadi tarehe 15 Septemba 2016 ili kujaza nafasi za udahili zitakazokuwa wazi baada ya uchaguzi wa awamu ya pili. Hatua hii itawezesha kuruhusu machaguo mapya kwa wale ambao hawakuchaguliwa katika kozi walizoomba pamoja na  kuruhusu waombaji wapya ambao kwa njia moja au nyingine hawakuomba udahili hapo awali.


Baraza pia linapenda kuwaarifu waombaji waliofanya maombi kwenye vyuo vya Ualimu vya Serikali kuwa uteuzi kwenye vyuo hivyo bado unasubiri mwongozo wa Serikali na hivyo watafahamishwa punde Baraza litakapopata mwongozo kutoka Wizara yenye dhamana ya Elimu juu ya uchaguzi huo. Waombaji wa vyuo hivi wanashauriwa kusubiri na kutokubadili machaguo yao hadi kutangazwa kwa uteuzi kwa vyuo vya Ualimu vya Serikali.


Aidha, Baraza linapenda kuwafahamisha waombaji wa Shahada ya Kwanza waliofanya maombi kupitia Mfumo wa Pamoja wa Udahili (CAS) wa Baraza kabla ya tarehe 16 Julai 2016 ambapo Tume ya Vyuo Vikuu ilitoa tangazo juu ya sifa za udahili na hawajafikisha sifa hizo kwamba unafanyika utaratibu wa kuwarudishia fedha zao. Utaratibu huu utamalizika baada ya kukamilisha tathmini ya idadi ya waombaji wa aina hiyo. Hivyo wahusika wanaombwa kuwa na subira  mpaka tathmimi itakapokamilika.

Imetolewa na
Ofisi ya Katibu Mtendaji
NACTE
Tarehe: 26 Agosti, 2016
Share:

0 comments:

Post a Comment