Tuesday, 4 July 2023

Fahamu Chimbuko la Wagner na harakati zake Russia.

 

Askari wa kundi la kivita la wagner wakiwa juu ya kifaru, wakati wa mapigano na Ukraine

Inaonekana kuna mzozo wa wazi kati ya kiongozi wa kundi hilo, Yevgeny Prigozhin na maofisa wa juu wa jeshi la Russia.

Ingawa ni mapema kusema mzozo huu utaisha lini, swali muhimu ni je, Prigozhin ni nani na ana nafasi gani katika kundi la Wagner?
Kundi la mamluki la Wagner lilianzishwa lini na nani? Kwa nini limekuwa tishio sana, hasa kwa Russia yenyewe?


Kundi la Wagner lina ofisi katika nchi 20 za Afrika, miongoni mwa hizo ni Eswatini, Lesotho na Botswana na lina wapiganaji katika nchi kadhaa duniani. Je, linapata wapi nguvu hizo?

Russia kundi hilo linajulikana kama ‘Kampuni ya Kijeshi ya Wagner’ (PMC). Ni kampuni binafsi ya kijeshi inayojumuisha mamluki na imefafanuliwa kama jeshi binafsi la Prigozhin ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais Putin wa Russia.

Kundi hili linafanya kazi hata nje ya sheria za Russia zinazopiga marufuku kampuni binafsi ya kijeshi.

Pia, inadaiwa kuwa huo ni mtandao wa jeshi la mamluki au jeshi binafsi la Rais Putin.
Kwa kuwa linafanya kazi kwa kuunga mkono masilahi ya Russia, linapokea vifaa, fedha na hata mafunzo kutoka Wizara ya Ulinzi ya Russia (MoD) na linasemekana ni Wakala wa Ujasusi wa Kijeshi wa Russia (GRU).

Kundi hili lilianzishwa mwaka 2014 na ofisa wa zamani wa GRU, Dmitriy Valeryevich Utkin, akishirikiana na mfanyabiashara Prigozhin. Lilikuja kujulikana zaidi wakati wa vita ya Donbas nchini Ukraine iliyoanza mwaka 2014 hadi 2015.

Mamluki hawa wameripotiwa kushiriki katika migogoro mingi duniani, hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mali.

Pia, mara nyingi hupigana upande wa vikosi vilivyounganishwa na Serikali ya Russia.
Wapiganaji wa Wagner wanatuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji, utesaji, ubakaji na unyang’anyi wa mali za raia.

Wagner amekuwa na jukumu kubwa katika uvamizi wa Russia nchini Ukraine, ambako iliwaandikisha katika jeshi lake wafungwa kutoka magereza ya Russia kwa ajili ya mapambano ya mstari wa mbele.

Miongoni mwa hao ni Mtanzania Nemes Raymond Tarimo (34), ambaye Januari mwaka huu aliripotiwa kuuawa wakati akipigana vita dhidi ya Ukraine akiwa upande wa jeshi hilo.

Wakati familia yake Tanzania ikisema haifahamu kilichompata kijana wao kwa kuwa wanachojua alikuwa masomoni Russia, walishangazwa kuona mitandaoni akiagwa kijeshi.

Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha wapiganaji kutoka Wagner wakiuaga mwili wa Tarimo, ambaye pia alipewa nishani baada ya kuuawa vitani katika shambulio la Bakhmut Mkoa wa Donbas mashariki mwa Ukraine.

Kuna madai yasiyothibitishwa kwamba Nemes alifungwa na baadaye alipewa nafasi ya kutoka jela kwa sharti la kujiunga na jeshi hilo, lakini familia ilisema haina taarifa za kwamba alikuwa jela wala kujiunga na jeshi, bali wanachokifahamu alikuwa mwanafunzi nchini humo.

Vyombo vya habari viliripoti Nemes alikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na dawa za kulevya Russia na aliambiwa angeachiliwa ikiwa atapigana vita Ukraine.

Desemba 10 mwaka jana, mwili wa mwanafunzi Mzambia, Lemekhani Nyirenda (23), aliyeuawa katika mapigano Ukraine baada ya kutoka katika kifungo Russia, ulirejeshwa Zambia kwa maziko.

Prigozhin alikiri alimsajili Nyirenda jeshini kutoka gerezani, akidai Mzambia huyo alikubali kwenda kupigana vita dhidi ya Ukraine.

Waandishi Eleonora Ardemagni na Federica Saini Fasanotti katika kitabu chao, ‘From Warlords to Statelords: Armed Groups and Power Trajectories in Libya and Yemen’, wameandika: “Kundi la Wagner, ambalo pia linajulikana kama PMC Wagner, ni kampuni binafsi ya kijeshi ya Russia … ni mtandao wa jeshi la mamluki au jeshi binafsi la Rais wa Russia Vladimir Putin.”

Desemba mwaka jana, John Kirby wa makao makuu ya jeshi la Marekani, Pentagon, alidai kuwa kundi la Wagner lina zaidi ya wapiganaji 50,000 Ukraine, wakiwamo zaidi ya mamluki 10,000 na wafungwa takribani 40,000.

Mwaka 2016, Wagner ilikuwa na wapiganaji takribani 1,000 na kufikia Agosti 2017 waliongezeka hadi 5,000 na ilipofika Desemba mwaka huo walikuwa zaidi ya 6,000.
Kundi hilo linasemekana lilisajiliwa nchini Argentina na lina ofisi huko Saint Petersburg, Russia na Hong Kong, China.

Novemba mwaka jana, Wagner ilifungua makao makuu mapya mashariki mwa Saint Petersburg.

Mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, Utkin, ambaye ni mkongwe wa Vita ya Kwanza na ya Pili ya Chechinia; hadi mwaka 2013 alikuwa luteni kanali na kamanda wa brigedi wa kitengo cha vikosi maalumu vya GRU na vingine kadhaa.

Baada ya kuachana na jeshi, mwaka 2013 alianza kufanya kazi katika Kundi la Usalama la Moran, ambalo ni kampuni binafsi iliyoanzishwa na maveterani wa kijeshi wa Russia na kujihusisha na operesheni ya usalama na mafunzo duniani kote.

Mwaka huohuo, wasimamizi wakuu wa Moran walihusika kuanzisha Kikosi cha Kislavoni chenye makao yake huko Hong Kong, kilichotafuta watu wa ‘kulinda maeneo ya mafuta na mabomba’ nchini Syria wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka 2021, ripoti ya Sera ya Kigeni ya Marekani ilibainisha kuwa asili ya jina Wagner haijulikani, wengine wanasema ni la kikundi linatokana na ishara ya simu ya Utkin “Wagner” iliyobuniwa na Mjerumani Richard Wagner ambaye Utkin anasemekana kuichagua kutokana na mapenzi yake kwa utawala wa aliyekuwa dikteta wa Ujerumani, Adolf Hitler.

Prigozhin (62) kutoka Jeshi la Wagner, alijipatia umaarufu kwanza kwa kumiliki kampuni za upishi na migahawa, kusambaza vyakula na vinywaji katika hafla rasmi za Serikali huko Kremlin.

Mojawapo ya picha zake zinazojulikana sana ni pale anapompatia chakula Rais wa Russia na baadaye alipewa jina la utani la ‘mpishi wa Putin’.
Prigozhin na Putin wote wanatoka St Petersburg, jiji la pili kwa ukubwa nchini Russia na wanajuana tangu miaka ya 1990, wakati Putin akifanya kazi katika ofisi ya meya wa St Petersburg na kutembelea mgahawa wa Prigozhin ambao ni maarufu kwa maofisa wa eneo hilo.

Biashara ya upishi ya Prigozhin ilistawi na kupewa kandarasi za Serikali, kutoa chakula kwa shule na hatimaye jeshi.

Mwishoni mwa mwaka 2019, kundi lilikuja na kile linachokiita ‘amri kumi za Wagner,’ za kulinda masilahi ya Russia daima na kila mahali, kuthamini heshima ya askari wa Kirussia, kupigana si kwa ajili ya pesa bali kupata ushindi na kupigana kila mahali ikibidi.
Kufahamu zaidi uhusiano wa kundi hili na Serikali ya Russia, tukutane kesho.

Chanzo: Mwananchi



Share:
Location: Tanzania

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment