Inapotajwa orodha ya vijana wanasiasa ambao nyota zao zilianza kung’ara katika Serikali ya Awamu ya Tano, Jokate Mwegelo ni miongoni mwao.
Ni kati ya wakuu wa wilaya vijana ambao wameonyesha uwezo kiutendaji na kuzidi kujenga imani kwa vijana, kwamba wanapopata nafasi wanaweza kufanya makubwa.
Machoni mwa wengi alianza kuonekana katika mashindano ya urembo, akitwaa mataji ya Miss Kurasini, Miss Temeke na hatimaye akaibuka mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha Miss Tanzania mwaka 2006.
Sanaa haikuishia hapo kwa Jokate, kwa kuwa alionekana pia kwenye filamu na muziki, baadaye akajitosa kwenye siasa.
Mwaka 2017 aliteuliwa kuwa Kaimu Katibu wa idara ya uhamasishaji na chipukizi ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Nafasi hiyo alidumu nayo kwa miezi 11, akaondolewa na kukaa benchi kwa miezi mitatu kabla ya jina lake kutajwa kwenye ‘mkeka’ wa wakuu wa wilaya walioteuliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli Julai 2018. Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.
Hatua zote alizopitia kwenye urembo, burudani na hata siasa alikuwa peke yake.
Hata hivyo, mwishoni mwa mwaka 2022, alipata mtoto ambaye kwa kiasi fulani amebadili taswira na mwenendo wa maisha yake.
Mwananchi ilifunga safari hadi Korogwe ambako ndiko anakohudumu sasa kama mkuu wa wilaya na kufanya naye mahojiano maalumu, akieleza mambo kadhaa kuhusu ujio wa mtoto, maisha yake kwa sasa na mtazamo wake kuhusu ndoa na familia.
Swali: Unawezaje kubeba majukumu ya kusimama katika nafasi zote kama mkuu wa wilaya na sasa ni mama wa familia?
Jibu: Hata mimi sijui nawezaje, ninachoona kuna siri kubwa Mungu aliiweka katika uumbaji na jinsi alivyotoa majukumu kwa viumbe wake. Kuna mambo yanatokea hata wewe unajiuliza nimewezaje, lakini ndiyo maisha yanaenda.
Najitahidi kuwa mama bora na kuzingatia malezi ya mtoto kwa sababu mwishowe malezi ya mtoto ni mama. Ingawa katika jamii zetu za Kiafrika jamii pia inasaidia kwenye kulea, baba, ndugu wapo kwa ajili ya kusaidia malezi. Najikuta siku zinakwenda kwa sababu mimi siyo mama wa kukaa nyumbani muda wote, ninafanya kazi ya kuwatumikia wananchi ambayo inachukua muda wangu mwingi na inawezekana pia wakati mwingine namuibia muda wake.
Swali: Ilikuwaje siku ya kwanza kuwa mama, uliipokeaje hatua hiyo?
Jibu: Nilifurahi kwa sababu nilitaka kuona kiumbe nilichokitengeneza kinafananaje. Siwezi kusema kama nilipanga kupata mtoto kwa wakati huu lakini ilivyotokea nikaona ni neema na mtoto ni baraka.
Nikawa na shauku ya kutaka kumuona amefananaje. Kila nikimuangalia naona amefanana na mimi kwa kiwango kikubwa, mambo yake anayofanya, michezo yake kwa kifupi nasikia raha na ninamshukuru Mungu kwa kunipa mtoto huyu.
Swali: Kulingana na majukumu yako suala la unyonyeshaji unalizingatia kwa kiasi gani?
Jibu: Kwa upande wangu namshukuru Mungu siku ya kwanza niliyojifungua niliweza kumnyonyesha mtoto, alipata yale maziwa ya kwanza ambayo ni muhimu zaidi kiafya na humsaidia mtoto kujenga kinga yake ya mwili. Suala la unyonyeshaji nalo nalizingatia, siku za mwanzoni nilikuwa napata muda wa kurudi nyumbani namnyonyesha. Hata hivyo, nilifanya utafiti mdogo na kupata njia mbalimbali za kuhakikisha mtoto anapata maziwa ya mama.
Swali: Wanawake wengi wa sasa kunyonyesha kwao siyo kipaumbele, unawaambiaje?
Jibu: Siku hizi teknolojia imerahisisha kwa kiasi kikubwa suala la unyonyeshaji, unaweza kukamua maziwa na kuyahifadhi vizuri ukaacha nyumbani mtoto akayatumia muda ambao haupo. Nilimtafuta rafiki yangu mmoja ambaye yeye ni mama wa watoto wanne nikitaka kujua njia mbalimbali za kuhakikisha mtoto anapata maziwa akaniambia maziwa yangu ndiyo bora zaidi kuliko ya kununua.
Swali: Imezoeleka watu maarufu kuwaweka wazi watoto wao kwenye mitandao ya kijamii, kwa nini kwako imekuwa tofauti?
Jibu: Siyo kwamba nimemficha au nitamficha siku zote, nimetaka niwe naye kwanza mimi nimu-’enjoy’ na wanafamilia kabla ya kumtambulisha kwa wanadamu wengine. Dunia ina mambo mengi, sikupenda mtoto wangu asemwe na watu, yaani waanze kumchambua hivi akiwa mdogo. Nikaona sina sababu ya kumuacha achambuliwe, wacha niwe naye mwenyewe kwanza na familia yangu, ikifika wakati watu watamuona. Siwezi kumficha siku zote kwa sababu mtoto lazima aende kliniki, kanisani, shule kwa hiyo hakuna namna nitamficha milele.
Swali: Kuna ugumu wowote kuwa mama?
Jibu: Hapana, maisha yana changamoto nyingi ila Mungu anatupa uwezo wa kuzipokea na kuzihimili. Mungu anatupa amani wakati wa mapito yote. Suala la kulea ni neema na baraka kutoka kwa Mungu. Daktari wangu aliniambia alikuwa akiona watu 20 hadi 30 kwa siku wakiwa na changamoto ya kupata mtoto, sasa ukipewa hiyo baraka ni muhimu uipokee.
Swali: Ulijisikiaje kuona kwenye mitandao ukizungumziwa wakati wa ujauzito wako?
Jibu: Kwangu ilikuwa kawaida, nimekaa kwenye tasnia ya kujulikana kwa zaidi ya miaka 15, kuna kitu gani kipya cha kunishtua. Mimi ni mtu ninayependa uhalisia, sikutaka kujificha maana wapo ambao wanaficha ujauzito ila sikuona haja ya kufanya hivyo
Nimetengeneza usugu unaonifanya nielewe kwamba kuna vitu vinapita na vingine vinabaki. Vile vinavyobaki ndiyo vya msingi, vinavyopita visikuhangaishe, katika hili kilichobaki ni mtoto na mwili wangu bado upo, ujauzito na kule kuvimba kumeshaondoka, kwa hiyo vitu vya kupita kama hivyo haviwezi kunisumbua.
Swali: Wewe ni mama wa aina gani?
Jibu: Mimi ni mama ambaye napenda mtoto ajifunze na aweze kujitegemea, siyo mama wa kudekeza mtoto. Nimeanza kumshikisha glasi nikimtengenezea mazingira ya yeye kujifunza kutambua mazingira yake. Mfano sasa hivi nimekataza asibebwe, nataka aachwe acheze, atambae, kwa kifupi ajitafute. Mimi ni mama ambaye nataka mtoto aanze kujitegemea taratibu, siyo kwamba nitakuwa mkali ila atajifunza kujitegemea mapema na atapata pia wakati mzuri.
Swali: Unataka mtoto wako awe kama wewe?
Jibu: Kwa kweli vile Mungu atataka awe ndivyo atakavyokuwa. Sisi kama wazazi tutakuwapo kwa ajili yake kuhakikisha tunaendeleza vipaji vyake, kumpa misingi mizuri na kumsaidia kujua kwamba dunia siyo rahisi bila kumtanguliza Mungu.
Swali: Nje ya ofisi, Jokate ni mwanamke wa aina gani?
Jibu: Licha ya kuwa kiongozi wa Serikali, mimi ni mwanamke, ninapokuwa nyumbani nabeba majukumu yote ya mwanamke na mama. Ninapopata wasaa napika, nafanya usafi na mambo yote ya nyumbani. Chakula cha mtoto huwa naandaa, namlisha, namuogesha na vitu vingine, kwa hiyo ukuu wa wilaya hauniondolei majukumu yangu kama mwanamke.
Swali: Vipi kuhusu mipango ya ndoa na baba wa mtoto wako?
Jibu: Suala la ndoa haulizwi mwanamke, ni mwanaume ndiye anafanya uamuzi, mkimpata baba mtoto wangu ndiyo muulizeni anaweza kuwa na majibu.
Mimi sijitolei posa wala mahari, hakuna mwanamke ambaye hapendi ndoa au familia, lakini kila kitu hutokea kwa wakati wake na kwa jinsi ambavyo Mungu ataelekeza. Ni utaratibu mzuri wa kimaisha kuwa na ndoa na familia lakini iwe kwa kadri ambavyo Mungu atajalia. Hivyo tuzidi kumuomba afungulie hiyo neema kwa sababu unaweza kukimbilia kitu halafu ikawa ni hasara.
Chanzo: Mwananchi Digital.
0 comments:
Post a Comment