Wednesday, 5 July 2023

Sudan Kusini kufanya uchaguzi wa kwanza tangu ipate uhuru.

 

Salva Kirr. Raisi wa sudan kusini

Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir amesema uchaguzi ambao ulichelewa kwa muda mrefu nchini humo utafanyika mwakani kama ilivyopangwa.

Hata hivyo Rais Kiir amesema atawania tena uchaguzi huo, wa kwanza tangu nchi hiyo kupata uhuru.

Mpaka sasa hakuna mgombea mwingine ambaye ametangaza kugombea lakini Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar ni miongoni mwa wanaoanatarajiwa kutangaza nia ya kugombea kinyang’anyiro hicho.


Rais Kiir amekuwa katika nafasi hiyo tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 2011 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu.

Hata hivyo mzozo uliendelea hata baada ya uhuru. Vita vya wenyewe kwa wenyewe viliibuka tena mwaka 2013 wakati rais Kiir alipokosana na Machar.

Makubaliano ya kugawana madaraka yalitiwa saini kati ya pande zinazozozana mnamo Agosti 2018 katika jitihada za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano.

Jukumu la serikali ya mpito ambalo lilipaswa kukamilika mwaka 2022, liliongezwa ili kuruhusu viongozi hao kutatua changamoto za utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Jumanne Julai 5, 2023 Rais Kiir alisema changamoto za amani zitashughulikiwa kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 2024.

Chanzo: Mwananchi

Share:
Location: Tanzania

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment