Wednesday 18 June 2014

Taarifa ya Uchaguzi wa Wanafunzi Kidato cha Tano 2014

TAARIFA:

Uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia Kidato cha Tano katika shule za  Serikali na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2014 umekamilika. Uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia takwimu za matokeo ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne Tanzania Bara mwaka 2013.

2.0 WATAHINIWA WALIOFANYA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE, MWAKA 2013

Jumla ya watahiniwa  427,679  walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013, wakiwemo wasichana  199,123  sawa na asilimia  46.56  na wavulana  228,556 sawa na asilimia  53.44.  Kati yao watahiniwa  404,083  sawa na asilimia  94.48  walifanya mtihani na watahiniwa  23,596  sawa na asilimia  5.52  hawakufanya mtihani huo.

2.1 Watahiniwa wa Shule (School Candidates)

Kwa Watahiniwa wa Shule, watahiniwa  367,163  walisajiliwa kufanya mithanikati yao wavulana ni  198,099  na wasichana ni  169,064.  ambapo  watahiniwa  352,614 sawa na asilimia  96.04  walifanya mtihani; kati yao wasichana walikuwa 162,412 sawa na asilimia  96.07  na wavulana  190,202  sawa na asilimia  96.01 . Watahiniwa 14,549  sawa na asilimia  3.96  hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.

2.2 Watahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidates)

Kati ya watahiniwa 60,516  wa kujitegemea waliosajiliwa kufanya mtihani, watahiniwa  51,469  sawa na asilimia  85.05 walifanya mtihani na watahiniwa  9,047  sawa na asilimia  14.95  hawakufanya mtihani kwa sababu mbalimbali.

Jumla ya watahiniwa  235,227  sawa na asilimia  58.21  ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2013 walifaulu. Mwaka 2012 watahiniwa waliofaulu walikuwa  185,940  kati ya  431,650  waliofanya mitihani; hii ni sawa na asilimia  43.08.  Matokeo haya yanaonesha kuwa mwaka 2013 ufaulu umeongezeka kwa asilimia  15.13.

3.1 Ufaulu wa Watahiniwa wa Shule

Mwaka 2013 Watahiniwa wa Shule waliofaulu ni  201,152  sawa na asilimia  57.05  ya watahiniwa  352,614  waliofanya  mtihani.  Kwa mwaka 2013 kuna ongezeko la ufaulu wa watahiniwa 41,405, sawa na asilimia 25.91 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2012 ambapo watahiniwa 159,747 walifaulu.

3.2 Ufaulu wa Watahiniwa wa Kujitegemea

Takwimu zimeonesha kuwa kumekuwa na ongezeko la ufaulu kwa watahiniwa wa kujitegemea kutoka  26,193,  sawa na asilimia  43.07  mwaka 2012 hadi kufikia watahiniwa  34,075,  sawa na asilimia  66.21  kwa mwaka 2013; Kwa kulinganisha na mwaka 2012 lipo ongezeko la asilimia  30.09 kwa ufaulu wa watahiniwa wa kujitegemea.

Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I -III umefikia watahiniwa  71,527  sawa na asilimia  20.28  ya watahiniwa waliofanya mtihani Tanzania Bara. Hivyo kuna ongezeko la ufaulu wa asilimia  106.73  ikilinganishwa na matokeo ya ufaulu kwa mwaka 2012, kwa kuwa watahiniwa wa shule waliofaulu katika madaraja I-III kwa mwaka huo walikuwa  34,599  sawa na asilimia  9.67  ya watahiniwa waliofanya mtihani.

5.0 TARATIBU ZA UCHAGUZI WA WANAFUNZI WA KIDATO CHA TANO 2014.

Kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali, mwanafunzi anayeomba kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kidato cha tano na vyuo vya Ufundi, hulazimika kujaza  ‘Selform'  ambayo ndiyo fomu rasmi ya maombi. Kwa kutumia fomu hiyo, mwanafunzi huchagua maombi  matano ya tahasusi (Combinations) za masomo anayotaka kusoma na shule anayotarajia kujiunga nayo kwa kila chaguo. Kamati ya uchaguzi humpanga mwanafunzi katika machaguo yake ya  masomo na shule kwa kuanzia na chaguo la kwanza. Kama mwanafunzi atakuwa hana sifa katika machaguo yote aliyoomba, mwanafunzi husika hupangiwa chaguo la somo alilofaulu zaidi na katika shule iliyopo karibu na wilaya yake ya makazi kulingana na tahasusi na nafasi zilizopo katika shule husika.

6.0 IDADI YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO

Jumla ya Wanafunzi  54,085  sawa na asilimia  75.61  ya wanafunzi  71,527  waliostahili kuingia Kidato cha Tano Tanzania Bara kwa mwaka 2014 wamechaguliwa; hilo ni ongezeko la wanafunzi  20,402  kwa kulinganisha na wanafunzi  33,683  waliochaguliwa mwaka 2013. Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 2014 wavulana ni  31,352 na wasichana ni  22,733.

Wanafunzi wamechaguliwa kujiunga kidato cha Tano katika jumla ya shule  241  zikiwemo shule  33  zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka 2014.

Nawashukuru sana wadau wote wa elimu katika Halmashauri mbalimbali kwa kuimarisha miundombinu ya shule hizo, ikiwemo maabara.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano 2014 ni kutoka shule za serikali na zisizo za serikali. Kati yao wavulana  14,826  sawa na asilimia 27.41 wamechaguliwa kusoma masomo ya  sayansi  na wavulana  16,526  sawa na asilimia  30.56  wamechaguliwa kusoma masomo ya  sayansi ya Jamii.  Aidha,wasichana  7,859  sawa na asilimia  14.53 wamechaguliwa kusoma masomo ya  sayansi  na wasichana  14,874  sawa na asilimia  27.50  wamepangwa kusoma masomo ya  Sayansi ya Jamii.

Nawapongeza walimu wote kwa juhudi walizozifanya katika ufundishaji kwa kuzingatia mbinu za ufundishaji walizopata kupitia mpango wa mafunzo kazini  (INSET) kwa walimu wa sayansi na lugha (Kiswahili na Kiingereza) unaosimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya WaziriMkuu, Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa. Aidha nawapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi. Hali hiyo inaonesha kuwa jitihada za Serikali za kuhamasisha vijana kusoma masomo ya Sayansi zimeanza kuzaa matunda.

Natoa wito kwa wanafunzi wa  jinsi zote  kujisomea kwa bidii masomo  yote, yakiwemo ya  Sayans i na  Sayansi ya Jamii , kwani yanategemeana. Walimu wa masomo ya Sayansi, Sayansi ya Jamii na Hisabati wanakumbushwa kutumia mbinu shirikishi za  kitaalam na kisaikolojia  katika kufundisha ili kuwavutia wanafunzi wengi zaidi kusoma na kufaulu mitihani yao. Aidha walimu wa masomo ya Sayansi, waendelee kuwahamasisha wanafunzi kusoma masomo ya Sayansi wakiwemo  wanafunzi wa kike . Aidha, wanafunzi wa kike wanapaswa kujiamini kuwa wanaweza masomo yote yakiwemo ya Sayansi, kwani siri ya kujifunza ni utayari.

7.0 WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA UFUNDI, MWAKA 2014

Jumla ya wanafunzi  472 wakiwemo wavulana  355 na wasichana  117 wamechaguliwa kujiunga na Vyuo vya Ufundi. Idadiya wanafunzi hao imepungua kutoka  530  mwaka 2013 hadi  472  mwaka 2014 kwa sababu kwa sasa vyuo hivyo vimeanza kuchukua wanachuo wa shahada ya kwanza. Aidha, kutokana na ufaulu kuongezeka idadi ya  wanafunzi wa kike  waliochaguliwa kujiunga na vyuo hivyo imeongezeka kutoka wanafunzi  114  mwaka 2013 hadi wanafunzi  117 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia  2.63.

Natoa wito kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii masomo ya sayansi ili mwakani idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi iongezeke ili Taifa lipate wataalam wa kutosha wa ngazi zote.

8.0  SABABU ZA WANAFUNZI KUKOSA KUCHAGULIWA KUINGIA KIDATO CHA TANO Jumla ya wanafunzi  16,800  wakiwemo  watahiniwa wa kujitegemea 10  waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo: ufinyu wa nafasi za shule za Kidato cha Tano (wanafunzi  16,400 ) na kukosa  tahasusi - Combination  (wanafunzi  400 ).

Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili baada ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia nafasi ya kusoma kidato cha Tano na cha Sita kwa pamoja na shahada ya Ualimu wanafunzi wenye sifa.

Shule za Kidato cha Tano na Sita zinatakiwa kuwa na mahitaji ya msingi, ikiwemo miundombinu yenye uwiano sahihi wa  vyoo, bafu, vyumba vya madarasa, bweni, jiko, bwalo, maktaba, maabara, chumba cha Jiografia ; pamoja na  samani  kulingana na idadi ya wanafunzi.

Shule zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Nne ambazo zinahitaji kuanzisha kidato cha Tano, zinatakiwa kuwa na miundombinu na mahitaji kamilifu yanayotosheleza kidato cha Kwanza hadi cha Nne kabla ya kuanza kujenga miundombinu ya Kidato cha Tano na Sita.

Natoa wito kwa Makatibu Tawala Mikoa wawaelekeze Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Majiji kuhakikisha azma ya Serikali ya kila Tarafa kuwa na shule ya Kidato cha Tano inatekelezwa ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaokosa nafasi. Kutokana na ongezeko la ufaulu wa masomo ya sayansi tunahimiza shule zitakazoanza Kidato cha Tano ziwe na maabara ili kuongeza idadi ya wanafunzi wa tahasusi za sayansi.

Aidha, shule ambazo hazikupangiwa wanafunzi kutokana na mapungufu mbalimbali, Makatibu Tawala wa Mikoa husika wanahimizwa kuwaelekeza Wakurugenzi kusimamia kwa karibu ukamilishwaji wa shule hizo ili ziweze kupokea wanafunzi wa chaguo la pili (Second selection).

Natumia nafasi hii kuwahimiza wadau wote wa Elimu kuhakikisha kuwa shule zote zinazoanzishwa kwa ajili ya kidato cha Tano ziwe za bweni kwa kuwa wanafunzi wa kutwa ni wachache na ni  lazima watoke eneo husika.  Kwa mfano, mwaka huu shule ya sekondari Buswelu ya mjini Mwanza imekosa wanafunzi kwa kuwa ni ya kutwa na Mwanza kuna shule 3 za kutwa. Hivyo ilikuwa vigumu kupata wanafunzi wa eneo hilo wa kutosheleza shule hizo.

Wakuu wa Shule  wahakikishe kuwa wanafunzi wa kidato cha nne wote wanajaza ‘Selforms' kwa umakini na kwa usahihi ili kurahisisha zoezi la uchaguzi. Aidha, wazazi kwa kushirikiana na walimu wawaelekeze watoto wao  kuwa na dira , kuwasaidia kusoma kwa malengo na kufanya machaguo ya tahasusi kulingana na dira walizonazo.

10.0 WANAFUNZI KURIPOTI KATIKA SHULE WALIZOPANGWA

Muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano mwaka huu 2014,utaanza  mwezi Julai tarehe 10 . Wanafunzi wamepangwa katika shule zenye miundombinu na walimu kwa masomo husika. Aidha, iwapo baadae mapungufu yatajitokeza, wakuu wa shule wameelekezwa kutoa taarifa kwa uongozi wa Halmashauri husika kuhusu upungufu huo.

Uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano umefanyika kwa kutumia mfumo wa kompyuta kwa kuzingatia machaguo ya wanafunzi pamoja na ufaulu hivyo hakutakuwa na mabadiliko yoyote. Kwa nafasi hii,  naagiza wanafunzi wote kuripoti katika shule walizopangwa tarehe 10 Julai, 2014 . Wanafunzi ambao watashindwa kuripoti shuleni hadi tarehe 30 Julai, 2014  nafasi zao zitajazwa na wanafunzi ambao wamekosa nafasi.

Mwisho ninachukua nafasi hii kuwapongeza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi mwaka 2014, walimu, wazazi, Bodi za Shule, viongozi, jamii na wadau wote wa elimu kwa jitihada za kuwaandaa wanafunzi, na kufanikiwa kuingia Kidato cha Tano. Ushirikiano wa wadau wote unatakiwa ili kuboresha elimu hapa nchini.

Wataalam wa elimu kuanzia ngazi ya shule wawe na utaratibu endelevu wa kuelimisha wadau katika utekelezaji wa malengo yanayopimika. Katika utaratibu wa ”Matokeo Makubwa Sasa  (Big Results Now)”;  kila mmoja anatakiwa  kuacha utendaji wa mazoea  na afanye kazi  kwa malengo na viwango , kuwa na  mipango inayotekelezeka  ya muda mfupi na muda mrefu na kuwa na  vipindi vya tathmini  kwa kila lengo kabla, kati na mwisho wa utekelezaji. Ni matumaini yangu kuwa wakuu wa shule na viongozi wote wa elimu wakizingatia taratibu hizi, elimu inayotolewa hapa nchini itaendelea kuwa bora zaidi.

Soma Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2014 hapa

Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Mhe. Kassim M. Majaliwa (MB)
OFISI YA WAZIRI MKUU - TAMISEMI
 
Share:

0 comments:

Post a Comment