Tuesday 22 July 2014

Bei ya umeme chini zaidi Tanzania


                                                 THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
                                                               Tokeo la picha la tanzania logo

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

Tanzania ndiyo nchi ambayo bei yake ya umeme ni ya chini zaidi miongoni mwa nchi zote wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameambiwa leo.
Pamoja na hali hiyo, Tanzania imedhamiria kuchukua hatua za kuzidi kupunguza bei hiyo, ili kuufanya umeme kuweza kupatikana kwa gharama nafuu zaidi na kwa uhakika zaidi kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika leo,
Jumamosi, Julai 19, 2014 mjini Mbinga na kuhutubiwa na Rais Kikwete, Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amemwambia Rais na wananchi kuwa Tanzania inauza uniti moja ya umeme kwa senti 16.8 tu za dola ya Marekani wakati nchi nyingine zilizobakia za EAC zinauza umeme wake kwa gharama kubwa zaidi.
Amesema kuwa Kenya inauza uniti moja kwa senti 18, Uganda inauza kwa senti 18.5 wakati Rwanda inauza umeme wake kwa senti 23 za dola ya Marekani.
Rais Kikwete na Waziri Muhongo wote wamesema kuwa pamoja na kwamba umeme wa Tanzania ni rahisi kuliko ilivyo katika nyingine zote za Afrika Mashariki, bado Serikali inaangalia hatua ambazo zitazidi kupunguza bei hiyo ili iwe ya chini zaidi na kunufaisha zaidi wananchi.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza kwenye ufunguzi wa Stendi ya Mabasi mpya na ya kisasa sana na kufungua barabara mpya ya lami ya kutoka Songea hadi Mbinga mjini Mbinga, Songea.
Rais Kikwete ameambiwa kuwa Stendi hiyo yenye vyumba 112 vya kisasa vya kufanyia biashara imejengwa kwa gharama ya sh. bilioni 2.17 ikiwa ni mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa (LGLB).
Akipata maelezo ya ujenzi wa barabara ya Songea-Mbinga, Rais Kikwete ameambiwa kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 78, imegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 64.3 na imegharimiwa na Serikali ya Marekani kupitia taasisi yake ya Millennium Challenge Corporation (MCC) na kampuni tanzu ya MMC ya Millennium Challenge Account Tanzania (MCA-T).
Kwa sababu ya hali ya milima na mabonde katika eneo ambako barabara hiyo inapita ujenzi wake umechukua miezi 39 badala ya 27 kama ilivyokubaliwa na ujenzi wake ulikamilika Januari 7, mwaka huu, 2014.
Ujenzi wa barabara hiyo ambayo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na hata wale wa nje ya Mkoa, ulihusika pia ujenzi wa madaraja makubwa katika mito minne likiwemo daraja kwenye Mto Ruvuma.
Baadaye, Rais Kikwete ameifungua rasmi Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mbinga iliyoko katika kata ya Kigonsera. Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka huu kwenye majengo yaliyokuwa yanatumiwa na watalaam waliojenga barabara ya Songea-Mbinga, ilifunguliwa mwanzoni mwa mwaka huu ikiwa na wanafunzi 60.
Shule hiyo ya bweni ya Serikali inafundisha masomo ya mchepuko wa sayansi tu na Rais Kikwete ameipongeza Wilaya ya Mbinga kwa kuanzisha shule hiyo akiutaka uongozi wa Wilaya ya Mbinga na halmashauri yake kuanza ujenzi wa majengo kwa ajili ya upanuzi wa shule hiyo mwakani ambako wanafunzi walioko kidato cha kwanza wataingia kidato cha pili.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
19 Julai, 2014
Share:

0 comments:

Post a Comment